Thursday, 5 January 2017

Mtama ni kundi la mbegu ndogo aina ya mazao ya nafaka au nafaka ambayo kwa jina la kisayansi unajulikana kama (Sorghum bicolor), ni mazao yanayolimwa sana duniani kote kwa ajili ya chakula na lishe.Mtama hutoa mazao mengi hata kwenye hali ambayo haifai kwa kilimo cha aina nyingine za mazao ya nafaka. Mtama una uwezo mkubwa wa kustahimili ukame.


Mtama unaweza kutumika kwa kuchemshwa na kuliwa kama ulivyo, kusagwa na kutumika kwa uji, kutengenezea vinywaji kama vile biakuoka mikate, na aina nyinginezo za vitafunwa. Mmea wa mtama pia hutumika kwa ajili ya malisho ya mifugo kama vile hay  na sileji. Mtama unastawi vizuri kwenye mazingira yenye wastani wa milimita 400 – 700 za mvua kwa mwaka. Pia mtama unavumilia sehemu zinazotuhamisha maji, na unaweza kulimwa sehemu zenye mvua nyingi.
Mtama unafaa pia kwa sehemu kame zenye wastani wa joto la chini kiasi cha nyuzi joto 18°C, ili kuweza kuota vizuri, na kiasi cha nyuzi joto 25-30°C ili kukua vizuri. Mtama hauwezi kuvumilia barafu. Mtama unaweza kukua kwenye aina zote za udongo. Kwa kiasi kikubwa unafaa zaidi kwenye udongo wa mfinyanzi, lakini pia kwenye udongo ambao una kiasi kidogo cha mchanganyiko wa kichanga. Mtama unaweza kuvumilia uchachu kwenye udongo kuanzia pH 5.0-8.5, na inavumilia udongo wenye chumvi kuliko yalivyo mahindi.
Aina za mtama
Kwa jumla kuna aina zaidi ya 30 za mtama zinazolimwa kama chakula. Mtama hustawi vizuri kwenye joto ikivumilia pia ukame. Hivyo ni nafaka muhimi kwenye maeneo yabisi za Afrika. Katika miaka ya nyuma kilimo chake kiliachwa mara nyingi kwa ajili ya mahindi kwa sababu mahindi huleta mazao makubwa zaidi kwa ekari. Lakini wakati wa ukame mahindi ni hasara na watu hurudi-rudi kwenye kilimo cha mtama.
Aina za mtama zinatofautiana kulingana na rangi zake, kuna nyeupe, nyekundu, na kahawia. Mbegu za asili huwa zinachavushwa kwa urahisi zaidi lakini mavuno yake huwa ni hafifu ukilinganisha na mbegu za kisasa. Hata hivyo, aina za kisasa zinazalishwa kwa gharama nafuu zaidi zinapopandwa kwa kufuata kanuni za kilimo bora.
Serena:  Ina punje za kahawia. Aina hii hustawi kwenye eneo lenye mvua za wastani na hukomaa katika kipindi cha siku 110. Aina hii huwa na shina na mizizi imara, ambapo huweza kuzalisha kiasi cha kilo 3,000 kwa hekari moja. Ambapo zinahitajika kilo 5 za mbegu kwa hekari moja. Aina hii ina uwezo wa kukabiliana na ugonjwa milia, kutu, na madoa ya kahawia kwenye majani.
Seredo:  Hii ni aina nyingine yenye punje za kahawia, na inapendekezwa Kulimwa kwenye eneo lenye mwinuko wa mita 1,500 kutoka usawa wa bahari. Aina hii huchanua baada ya siku 71 na hukomaa katika kipindi cha siku 120. Aina hii huwa ni ndefu, na ina uwezo wa kuzalisha kilo 5000 kwa hekari moja. Ina uwezo wa kukabiliana na ugonjwa wa milia, kutu, mabaka kwenye majani, na madoa ya kahawia kwenye majani.
Gadam: Inafanya vizuri katika sehemu ambazo si kame sana. Katika nchi nyingi mfano Kenya, aina hii ya mtama hutumika kutengenezea bia na pia kwa chakula. Aina hii huvumilia bungo na ugonjwa wa majani.
Hakika na Wahi:  Hizi ni aina mbili za mtama ambazo zimezalishwa na kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Ilonga kwa ajili ya kuoteshwa kwenye mashamba yalioathiriwa na viduha. Mbegu hizi zina rangi ya manjano iliyopauka. Unga wa aina zote mbili zinafaa sana kwa kupika ugali.
Utayarishaji wa shamba
Tayarisha shamba ili udongo uwelaini kurahisisha uotaji. Kama shamba limelimwa na trekta inabidi lipigwe haro na ikiwa limetayarishwa kwa jembe la mkono, mabonge mabonge ya udongo yanatakiwa yavunjwe
Kiasi cha mbegu Upandaji kwenye mistari pasipo kupungizia kunahitaji kilo 7 hadi 8 kwa hekta na upandaji kwa mashine unahitaji kilo 8 hadi 10 kwa hekta.
Upandaji Unaweza kupanda kwenye vumbi kabla ya mvua kunyesha, au wakati mvua zinapoanza au , wakati mvua zimenyesha za kutosha. Kina: Kupanda kwenye vumbi cm 5.0 – 6.0; Kupanda kwenye udongo wenye unyevu cm 2.5 – 4.0 Nafasi: Sehemu za unyevu mwingi: 60cm x 20 cm (cm 60 kati ya mstari na mstari na cm 20 kati ya shina na shina); Maeneo makame : cm75x cm20 au cm 90 x cm30 .
Mbolea:
Aina mbalimbali za mbolea na samadi zinatumika kuongeza rotuba ya udongo Samadi: Inatakiwa isambazwe kwenye shamba na kulimiwa chini au iwekwe kwenye mistari na kuchanganywa na udongo kabla ya kupanda. Kiasi kilichopendekezwa ni tani 5-10 kwa hekta na iwekwe mwezi mmoja kabla ya kupanda. Mbolea Kabla ya kupanda:
Mbolea aina ya DAP, 20:20:0, 23:23:0 katika kiwango cha kilo 20kg N na ~ 20 kilo P2O5 kwa eka, iwekwe wakati wa kupanda na kabla ya kupanda mbegu . Top dressing: Kilo 20 N za mbolea aina ya Urea, CAN. Iwekwe pemebeni mwa mimea na hakikisha inawekwa wakati kuna unyevu wa kutosha wa kuyeyusha mbolea vizuri
Palizi:
Palizi lifanyike mara mbili. Palizi la kwanza lifanyike wiki 2-3 baada ya mbegu kuota. Dawa za kuua magugu zinazowe za kutumika ni aina ya Lasso au Gesaprim (kabla ya kuota) na 2,4 D (baada ya kuota).
Kupunguzia
Mimea ipunguziwe ikiwa na wiki 3-4 baada ya kuota na ipunguziwe wakati udongo una unyevu wa kutosha kupunguza madhara kwa mimea.
Wadudu Waharibifu:
(i) Inzi wa bua (Antherigona soccata) Madhara yanatokea siku 7 hadi 30 baada ya kuota . Viluwiluwi wanakula ndani ya mmea na kusababisha dalili za moyokufa (deadheart). Ucheleweshaji kupanda huongeza madhara .
(ii) Vitoboa-bua (Stem borers Chilo partellus) Dalili ni vidirisha vidogo kwenye majani machanga . Viluwiluwi hutoboa bua na mimea michanga inaonyesha moyokufa (deadhearts).
Kuzuia
• Kupanda mapema
• Kuondoa na kuchoma mabua ya msimu uliopita
• Kutumia mbegu zenye ustahimilifu
• Kutumia madawa ya kunyunyizia kama vile aina ya chembechembe za Bulldock inayowekwa kwenye mimea ya umri wa wa wiki 4 kuzuia “vitoboabua”
Wadudu waharibifu wa masuke na punje
(i) Sorghum midge (Contarina sorghicola) Madhara huletwa na viluwiluwi wanaokula ndani ya kiini cha mbegu punjena kuzuia ukuaji wa mbegu na kuleta mapepe ya mbegu
Kuzuia: 
Upandaji mapema na kwa wakati mmoja wa mtama kwenye eneo kubwa • Mbegu bora za mtama /au chotara za mtama zinazostahimili madhara • Matumizi ya madawa kama Endosulfan, Ambush, Marshal au Karate.
Wadudu hifadhi
Wadudu muhimu katika maghala ya kuhifadhia mtama ni kama bungua na nondo.
(i) Bungua-mahindi ( Sitophilus zeamais) na Bungua mtama – Sitophilus oryzae). Bungua na viluwiluwi huharibu mbegu na kuifanya isiwe na matumizi yoyote .
Kuzuia 
Kuvuna mapema • Kukausha kikamilifu • Kutumia maghala ya kuhifadhia yenye ubora na ambayo yanapitisha hewa vizuri • Kusafisha ghala na kuweka dawa wiki 6 kabla ya kuvuna. Nyunyizia dawa kama vile Actellic Super, Malathion au pyrethrum dust.
Ndege
Kuna ndege kama quelea quelea, vile na njiwa.
Kuzuia 
Kupanda mapema mbegu zinazokomaa wakati mmoja katika maeneo ya karibu karibu.
• Kutumia nyaya za miali kama vile ribbons, aluminum foils, kanda .
• Mikebe ya mawe iliyofungwa na kamba ili kutoa sauti wakati kamba ikivutwa
• Kuvuna wakati unaofaa
• Kuharibu maeneo ya kuzaliana ndege
• Kutumia aina za mitama zenye uchachu.

0 comments:

Post a Comment

TANGAZA NASI KWA BEI NAFUU

TANGAZA HAPA

Powered by Blogger.

TANGAZO TANGAZO

TUNATENGEZA MACHINE ZA INCUBATOR KWA BEI POA.
HII NI OFA KWA AJILI YA MWAKA MPYA 2018. KARIBUNI SANA.

Video

Popular Posts

Our Facebook Page